Featured

ng’ombe wa maziwa bora zaidi kufuga kwa lengo la kuzalisha ni hawa hapa

Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa, unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti.
Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga. Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji.

Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya lishe na mambo mengine yako sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima kuzalisha kulingana na umbile lake na uwezo wake kamili. Kama utaweza kumudu kufuga ng’ombe halisi wa maziwa, ni lazima pia utambue kuwa uzalishaji wa juu wa maziwa uhitaji pia usimamizi wa hali ya juu. Kwa maana hiyo, ni vyema kufuga ng’ombe wa kiwango cha kawaida (ikiwezekana chotara) ambaye ataendana na uwezo wako wa kumtunza.


Ni vyema tukaangalia aina mbili za ng’ombe wa maziwa ambao wana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi;

(i) Freshiani (Friesian)

 
Ng’ombe aina ya freshiani ni rahisi kumtambua kutokana na kuwa na rangi nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama hawa ni wakubwa na pia wanaweza kuwa na mabaka meupe na meusi au mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa vizuri, freshian aliyefikia umri wa kukomaa huwa na uzito wa hadi kilogramu 550 na urefu wa sentimeta 150 kutoka begani. Mtamba huweza kupandwa, akiwa na umri wa miezi mitano huku akiwa na uzito wa kilogramu 360.


Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo wa kuishi kwa muda mrefu, uwezo wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni miaka sita. Hata hivyo, aina hii ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa maziwa ambao huweza kuzalisha kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa siku 360 yakiwa na kiwango cha chini cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ya ng’ombe.


Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji ulishaji mkubwa hivyo hushauriwa kwa wafugaji wenye uhakika wa kuwa na lishe bora na ya kutosha kwa mwaka mzima.

(ii) Ayrshire
 
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany). Ng’ombe hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540 katika umri wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si rahisi kupata matatizo yeyote ya miguu.
Ayrshire huweza kufanya vizuri katika malisho ya aina yeyote tofauti na aina nyingine ya ng’ombe wa maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri na ulishaji mzuri, wastani wa uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa na kiwango cha juu cha mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni aina nzuri kwa kufuga hasa kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na uzalishaji mkubwa wa maziwa. Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa na umbo zuri pamoja na chuchu zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha, utungaji wa maziwa yake, umefanya maziwa yake kuonekana ni mazuri sana katika uzalishaji wa siagi na jibini.
Maziwa ya Ayrshire yanafahamika kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na uwezo wake wa kuwa na mafuta ya kutosha na kiasi kikubwa cha protini. Kwa mfugaji anayeanza, aina hii ya ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo kasha baadaye kuongeza freshiani baada ya uwezo wako wa kuhudumia kuwa imara. Mifugo ya asili ni ghali sana na ni ngumu pia kuwapata, hivyo basi, njia rahisi kwa wafugaji wa maziwa wanaoanza ni kutafuta ng’ombe bora wa kawaida ambao mara nyingi huwa ni chotara, kisha kuwaboresha kwa kutumia mbinu ya kupandikiza dume bora na mwenye uzalishaji mkubwa. Na hii huhitaji elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi wa madume.


*Muhimu: Wakati wa kununua ng’ombe kwa ajili ya kufuga, ni vyema mfugaji ukatambua kuwa, wazalishaji wa maziwa mara nyingi hawauzi ng’ombe wao wenye uzalishaji mzuri, badala yake huuza wale ambao hawazalishi kwa kiwango kizuri, wale wenye matatizo kama kutokushika mimba, wenye matatizo ya joto na wale ambao hushambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Kwa maana hiyo, pamoja na aina ya ng’ombe unayehitaji kununua, ni muhimu sana kuwa mwangalifu usije ukanunua ng’ombe mwenye shida yoyote kwani hapo ndipo mwanzo wa uzalishaji wako kuja kuwa wa matatizo na kutokufikia lengo.

Subscribe to this Blog via Email :

2 comments

Write comments
JIMMY
AUTHOR
January 22, 2017 at 12:24 PM delete

Nashukuru kwa elimu yako, nami ninatarajia kuanza ufugaji na biadhara hiyo ya ng'ombe wa maziwa. Je, ni wapi naweza kupata mbegu bora na kwa bei gani?

Reply
avatar